MWANAMUZIKI nyota wa muziki wa Kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu kwa jina la Diamond ameibuka tena kinara wa Tuzo za Muziki za Kilimanjaro (KTMA) baada ya kujishindia tuzo tatu tofauti kwa mwaka 2012.
Diamond ameshinda tuzo hizo usiku huu katika Mkumbi wa Mlimani City baada ya kuibuka na tuzo ya Mtumbuizaji Bora wa Kiume, Mtunzi Bora wa Nyimbo na msanii ambaye ametoa Video Bora ya Muziki kwa mwaka huu.
Wimbo wa mwanamuziki huyo nyota ulioshinda katika tuzo hizo ni ‘Moyo Wangu. Hii ni mara ya pili ambapo Diamond anaibuka kinara wa mashindano ya KTMA, kwani mwaka juzi pia alikuwa msanii wa kwanza aliyejinyakulia tuzo nyingi zaidi.
Mwanamuziki Diamond akipiga picha na mama yake wa pili kutoka kushoto na Mkurugenzi wa ASET Asha Baraka kutoka kulia pamona na wanenguaji wake mara baada ya kupokea tuzo yake ya Mtunzi Bora wa Nyimbo.
Katika tuzo hizo wanamuziki walioshika nafasi ya pili kwa kujinyakulia tuzo mbili ni watatu wote kutoka muziki wa kizazi kipya, ambao ni Suma Lee, Ommy Dimpoz na Roma. Suma Lee ameshinda tuzo ya Afro pop (akunaga) na wimbo bora wa mwaka, Ommy Dimpoz ameshinda tuzo ya msanii bora anayechipukia na wimbo bora wa kushirikiana, huku Roma akijinyakulia tuzo ya mwanamuziki bora wa Hip Hop na wimbo bora wa Hip Hop.
Wasanii wengine ambao wamejinyakulia tuzo moja moja katika KTMA na tuzo zao kwenye mabano ni pamoja na Hadija Kopa (Mtumbuizaji Bora wa Kike), Janguar (Wimbo Bora wa Afrika Mashariki), Judith Wambura-Jay Dee (Muimbaji Bora wa Kike), Barnabas (Muimbaji Bora wa Kiume), Ben Paul (Mwanamuziki Bora wa R & B), Isha Ramadhan (Wimbo Bora wa Taarab), A.T (Wimbo Bora wenye vionjo vya Asili) na rapa Kanjo Kitokololo (aliyeshinda tuzo ya Rapa Bora wa Bendi).
Wengine walioshinda katika tuzo hizo ni pamoja Bendi ya Twanga Pepeta (Wimbo Bora wa Kiswahili), Manek kutoka A.M Records (tuzo ya Mtayarishaji Bora wa mwaka). Wanamuziki King Kiki na Marehemu Dk. Remmy Ongala pamoja na Taasisi ya JKT wameshinda tuzo ya kutoa mchango mkubwa katika tasnia ya muziki.