Tumezoea kuwaona watangazaji na waendesha vipindi vya televisheni maarufu kama vile Oprah Winfrey na kipindi chake Oprah Winfrey Show na Tyra Banks na kipindi chake The Tyra Banks Show wote hawa wakiwa ni wanawake wa Kiafrika wenye asili ya Marekani waliofanikiwa na kujizolea umaarufu kutokana na vipindi vyao hivyo.
Pamoja na kuwa ni Wamarekani weusi, lakini bado tukiwa kama Watanzania hatuwezi kujitapa ama kujivunia sana pamoja kwamba kwa asili wana damu ya Kiafrika.
Sporah akiwa na alikiba pamoja na Mims.
Lakini sasa huenda umefika wakati wetu nasi kujivunia watu wetu, watangazaji wetu, Watanzania wenzetu ambao wameamua kuvunja ukuta na kujitosa katika uendeshaji wa vipindi ama maonesho ya televisheni kama ilivyo kwa Oprah na Tyra.
Tuna kila sababu sasa kama watanzania kujivunia kwa sababu tumepata Mtanzania mwenzetu ambaye ameamua kuendesha kipindi cha mazungumzo katika televisheni, na huyu si mwingine bali ni Irene Sporah Njau ambaye ameanzisha Kipindi cha Majadiliano cha Kiafrika kinachojulikana kama The Sporah Show akiwa nchini Uingereza.
Irene Sporah Njau.
Kama hiyo haitoshi, binti huyo kutoka Tanzania ambaye hujulikana zaidi kwa jina la Sporah kuanzia Juni 11 The Sporah Show itakuwa ikioneshwa hapa nyumbani kupitia kituo kimojawapo cha televisheni nchini katika siku za Ijumaa na Jumamosi
"Kwa kweli TV Show ilikuwa ni ndoto yangu, ila nilipofika Uingereza na kuona jinsi ambavyo nchi za wenzetu zina mifumo tofauti ya kuelimisha jamii, nilijikuta vikinipa motisha zaidi ya kutaka kutimiza ndoto yangu ndipo nilipopata wazo la kuanzisha kipindi cha The Sporah Show" asema Irene Sporah Njau.