MWANAFALSAFA wa mashairi ya muziki nchini Hamisi Mwinjuma almaarufu kama Binamu au Mwana FA, ameamua kutoa albamu yake kwa mashabiki baada ya kukacha hilo kwa miaka miwili kwa kile alichokiita kusambaa kwa wizi wa albamu za wasanii nchini.
Binamu ambaye anawashauri watu wasije mjini huku yeye akiendelea kula bata jijini Dar es Salaam, amesema kwa sasa yupo tayari kuachia albamu hiyo ambayo anadhani itakuwa ni zawadi tosha kwa mashabiki wake.
"Ninatoa albamu kama zawadi kwa mashabiki, kwani ni muda mrefu sijafanya hivyo, ninaamini kuwa nitakapoitoa mashabiki watapata fursa ya kuzisikia nyimbo zangu nyingi ambazo hata hivyo hazijaweza kusikika redioni hata katika televisheni" alisema.
FA ambaye alianza muziki mwaka 1993 aliwahi kupata tuzo kadhaa za muziki na ametamba na singo kama ‘Alikufa Kwa Ngoma,'Habari Ndiyo Hiyo' na 'Binamu'.