Waandamanaji wakiwa na mabango yanayoezea jumbe mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) kwenye matembezi ya hisani yaliyoandaliwa na Mfuko wa maendeleo kwa Albino (BADEF) yaliyoanzia viwanja vya Leaders hadi Mnazi mmoja , Dar es Salaam jana.
Mwenyekiti wa Mfuko Mfuko wa maendeleo kwa Albino (BADEF) Salum Barwan akizungumza kwenye kampeni ya kusaidia Albino katika viwanja vya Mnazi mmoja , Dar es Salaam jana. Kulia ni Mstahiki Meya wa Kinondoni Yusufu Mwenda, kushoto, Mbunge wa viti maalum wa Tanga, Al-Shaymaa John.
Mstahiki Meya wa Kinondoni Yusufu Mwenda akizungumza kwenye kampeni ya kusaidia Albino katika viwanja vya Mnazi Dar es Salaam jana, kushoto ni Mbunge wa viti maalum wa Tanga, Al-Shaymaa John, kulia,Mwenyekiti wa Mfuko Mfuko wa maendeleo kwa Albino (BADEF) Salum Barwan.
LICHA ya kupungua kwa mauaji ya walemavu wa ngozi (Albino) nchini walemavu hao bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali kama ikiwemo ukosefu wa taarifa sahihi, dhana tofauti za ulemavu, saratani ya ngozi, elimu na ajira.
Imeelezwa kuwa licha ya kuwepo taasisi nyingi ambazo zinashughulikia matatizo yao, walemavu wa ngozi bado wanaendelea kukabiliwa na changamoto hizo, hivyo juhudi za ziada zinahitajika ili kuzitatua.
Akizungumza katika kilele cha matembezi ya hisani yaliyofanyika toka viwanja vya Leaders na kuishia viwanja vya Mnazi Mmoja mweneyekiti wa Mfuko wa maendeleo ya watu wenye ulemavu wa ngozi Barwany Albinism Development Trust Fund (BADEF) Bw Salum Barwany alisema kuwa taasisi na mifuko mingi iliyoanzishwa kwa ajili ya kushughulikia mambo yanayowahusu albino nyingi vimeweka kipaumbele mauaji kuliko kushughulikia changamoto nyingine.
Alisema kuwa ili kuweza kuwasaidia wamavu wa ngozi ni vyema taasisi na mifuko hiyo kutilia mkazo katika kutoa matibabu ya saratani ya ngozi kwa albino ambayo inaghalimu maisha ya walemavu pamoja na kutoa elimu juu ya ulemavu wa ngozi kwa jamii.
“Wengi wanatazama matukio ya mauaji kuwa ndio kigezo na kipimo , lakini ukweli ni kwamba mauaji yanayoendelea nchini dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi ni sehemu tu ya tatizo lakini matatizo yako mengi na ya kutisha zaidi ambapo juhudi za makusudi zinahitajika kuzikabili,” alisema Bw Barwany
Mwenyekiti huyo alifafanua kuwa ukosefu wa taarifa sahihi ni moja ya changamoto kuu ndani ya jamiii ya watanzania juu ya dhana ya ulemavu wa ngozi pamoja na huduma kwa watu wenye ulemavu wa ngozi nazo ni mgogoro.
Barwany ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Lindi mjini alisema kuwa kupitia mfuko wake wamezindua kampeni inayojulikana kama ‘Nifahamu’ ambayo nia yake ni kuendesha tafiti za kitaalam ili kubaini changamoto za kielimu, za afya, na za malezi kwa kitaalamu na kwa undani zaidi.
Akizungumza na baadhi ya walemavu wa ngozi pamoja na wadau mbali mbali waliohudhulia katika matembezi hayo kwa niaba ya Waziri wa afya na ustawi wa jamii Dk Hadji Mponda, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam Bw Yusuph Mwenda alisema kuwa kuanzishwa kwa mfuko huo utamaliza baadhi ya changamoto zinazowakabili walemavu.
Alisema kuwa serikali kupitia wizara ya afya itaendelea kuchukua hatua mbali mbali kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavvu wa ngozi wanapewa tiba ya kansa ya ngozi kupitia wilaya kote nchini pamoja na hospitali ya saratani ya Ocean road na KCMC.
“Pamoja na kuwapatia huduma hiyo ya tiba wizara imeanza kutekeleza utaratibu wa kusamabaza mafuta ya kuzuia mionzi yajulikanayao kama Sunscreen lotion ambayo yanasambazwa katika hospitali zote za wilaya kupitia bohari ya dawa,” alisema.
Dk Mponda aliwataka walemavu wa ngozi katika mchakato wa kuandaa katika mpya washiriki kikamilifu katika kutoa maoni ili masuala ya watu wenye ulemavu yazingatiwe na pia watumie fulsa ya kujitokeza katika zoezi la sense ya watu na makazi ambayo itakusanya takwimu za walemavu nchini.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi Al-Shaymaa Kwegyir aliwata walemavu wa ngozi wajikinge na jua kutokana na ukweli kwamba saratani ya ngozi kwa walemavu hao kwa kiasi kikubwa inasababishwa na jua.
“Ninawaomba ndugu zangu msitembee katika barabara bila kujikinga na jua kwa sababu ni chanzo cha saratani hiyo na pindi mnapoona dalili yoyote hata ya kipele mfiike kwa wataalamu wa afya ili wawapatie tiba mapema kabla ugonjwa huo haujawa mkumbwa,” alisema.