Wasanii Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na 2face Idibia wa Nigeria Jana usiku wameibuka vinara wa tuzo za MaMa’z kwa mwaka 2010 baada ya kujinyakulia jumla ya tuzo mbili kila mmoja.
Wasanii hao walikuwa wanawania tuzo zaidi ya tatu katika vipengele tofauti na baadaye kujinyakulia tuzo za Video bora. Msanii bora wa Francophone ilienda kwa Fally Ipupa wakati 2Face akibeba Msanii wa mwaka na msanii bora wa kiume.
Sherehe hizo za kuwatuza wasanii wa kiafrika zilianza mida ya saa moja jioni ambapo wasanii mbali mbali pamoja na wageni waalikwa waliwasili katika eneo la Red Carpet kabla ya kupiga picha na kujipatia vinywaji vilivyokuwa tayari kabisa kwa ajili ya wageni hao.
Msanii wa Tanzania Diamond aliondoka mikono mitupu licha ya kupata nafasi ya kuimba pamoja na P-Unit na Teargas katika jukwaa moja.
Aidha sherehe hiyo zilianza rasmi majira ya saa tatu na nusu ambako msanii kutoka Marekani Rick Ross alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuamsha nderemo, vifijo na kelele za kutosha ukumbi mzima kabla ya kutoa fursa kwa tuzo ya kwanza kabisa kutolewa ambayo ilikuwa video bora iliyokwenda kwa Fally Ipupa.
Wasanii wengine waliopiga shoo ni pamoja na Moze Radio na Weasle, Jozi, Big Nuz, Sasha, Cabo Snoop, Barbara Kanam, Fally Ipupa, J Martins, 2 Face, Wande Coal, T-Pain, Mo Cheddah na Eve.
Baadhi ya watu maarufu waliokuwemo katika tuzo hizo ni pamoja na mchezaji wa mpira J J Okocha, Tatiana Durao, Munya na mmiliki wa kituo hicho cha televisheni cha MTV, Bw. Tedd Turner.
Sherehe hizo za kutuza wasanii wa kiafrika za MAMAs zimeletwa kwenu kwa udhamini wa Airtel, Master Card, Halmashauri ya Jiji la Lagos pamoja na hoteli ya nyota tano Eko Suites ambako ukumbi wake wa Eko Center ulitumika.