Wasanii Ambwene Yesaya `AY`’ kutoka Tanzania, Ngoni kutoka Uganda na Amani wa Kenya, wanatarajiwa kuonyeshana kazi jijini Dar es Salaam kesho katika tamasha maalum la muziki lililopewa jina la 'East African Bash' na kushirikisha nyota wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashairiki.
AY na wakali wenzake hao, watachuana kwenye ukumbi wa Da’ West uliopo Tabata na baada ya hapo, watachuana tena katika onyesho la pamoja litakalofanyika siku moja baadaye kwenye eneo la ufukwe wa Mbalamwezi jijini Dar.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, AY ambaye ni mmoja wa washiriki, alisema amejipanga kuwawakilisha vyema Watanzania kwa kuonyesha kiwango cha juu na kuwaduwaza wanamuziki kutoka Kenya na Uganda.
"Najua hili ni tamasha kubwa na mimi ndiye niliyebahatika kuwa mwakilishi pekee wa Tanzania… kwa sababu hiyo, nataka kufanya kweli ili kuwakilisha vyema," alisema AY.
Kwa upande wake mratibu wa tamasha hilo, Dennis Busulwa, alisema kuwa lengo kubwa la tamasha hilo ni kuendeleza umoja wa wanamuziki wa nchi za Afrika Mashariki.
0 comments:
Post a Comment